Savara na Barnaba kushirikiana kikazi

Savara aliwasili jijini Dar es Salaam jana ambako alipokelewa na Barnaba Classic.

Marion Bosire
2 Min Read
Savara Mudigi, Mwanamuziki wa Kenya

Mwanamuziki wa Kenya Savara Mudigi na mwenzake wa Tanzania Barnaba Classic wanatarajiwa kushirikiana kikazi kufuatia mkutano wao nchini Tanzania.

Savara ambaye ni mmoja wa waliokuwa wanachama wa kunsi la muziki la Kenya sauti Sol aliwasili nchini Tanzania jana ambapo alipokelewa na Barnaba katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walizungumza na wanahabari ambapo Savara alielezea kwamba aliposhirikiana na Dulla Makabila msanii wa mtindo wa Singeli nchini Tanzania, Makabila alimfahamisha kuhusu Barnaba akihimiza ushirikiano.

Alisema kwamba lengo kuu la ziara yake nchini Tanzania ni kufanya kazi za muziki na Barnaba, kama kurekodi nyimbo pamoja na kutengeneza video.

Mudigi alielezea pia kwamba dhamira yao ni kuendeleza na kukuza muziki wa Afrika Mashariki ili uweze kufikia viwango vya kimataifa na kuvutia hadhira pana zaidi duniani.

Barnaba kwa upande wake alisema kwamba ushirikiano huo kati ya Kenya na Tanzania utaleta taswira mpya katika tasnia ya muziki, na kuongeza kuwa kupitia juhudi hizo za pamoja, Wasanii wa Afrika Mashariki wataweza kushindana katika soko la kimataifa na kuonesha ubunifu pamoja na utamaduni wa kipekee wa ukanda huo.

Hatua hii inajiri wakati ambapo msanii mwingine aliyekuwa mwanachama wa Sauti Sol kwa jina Bien Barasa anazungumziwa sana nchini Kenya na Tanzania kufuatia kazi mpya aliyofanya kwa ushirikiano na msanii wa Tanzania Ali Kiba.

Share This Article