Sarah Hassan kuwa mgeni wa heshima wa kongamano la wanawake jijini Brazzaville

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji tajika wa Kenya Sarah Hassan ametangaza kwamba amealikwa kama mgeni wa heshima kwa kongamano kuhusu kuwezesha wanawake na maendeleo endelevu jijini Brazzaville katika Jamhuri ya Congo.

Kulingana naye kongamano hilo litaandaliwa katika hoteli ya Radisson Blu Machi 8-9, 2025.

“Hafla hii ya kipekee itawaleta pamoja wanawake wafanyabiashara, wataalamu na viongozi kutoka ulimwengu wa kiuchumi kubadilishana mawazo na kujenga ushirikiano.” aliandika Sarah kwenye Instagram.

Alisema ni wakati mwafaka wa kushabikia usawa wa kijinsia na kuhimiza maendeleo jumuishi yanayonufaisha wote.

Mwaliko wake ni kwa kampuni zote bila kuzingatia sekta, ili zihusike katika mchakato huo. “Kujitolea kwenu ni muhimu katika kubadilisha jamii na kuimarisha usawa.” aliandika Sarah.

Sarah anaonekana kupiga hatua kimataifa, siku chache baada ya kuangaziwa na jarida la Forbes Africa, ambalo huchukuliwa kuwa la hadhi ya juu.

Huwa linaangazia watu wa bara Africa waliobobea kwenye nyanja mbali mbali kama vile biashara, uwekezaji, teknolojia, ujasiriamali, uongozi na hata mitindo ya maisha.

Share This Article