Usimamizi wa timu ya soka ya Shabana FC umemteua Sammy Omollo maarufu kama Pamzo kuwa kocha wa timu hiyo.
Uteuzi huo ulifanywa kupitia kwa taarifa ambayo ilisema kwamba ujio wa Omollo ni jambo la kufana ikitizamiwa ujuzi alionao na uzoefu katika kazi hiyo.
“Mapenzi yake kwa mchezo wa soka na kujitolea kwake kunoa talanta za wachezaji ni vitu ambavyo vinawiana na maono ya timu ya Shabana,” ilisema taarifa hiyo.
Omollo anachukua mahali pa kocha Sammy Okoth ambaye alijiuzulu mwezi Oktoba mwaka jana baada ya Shabana kushindwa mabao manne kwa sifuri na Ulinzi Stars.
Okoth wakati huo alitetea hatua yake ya kujiuzulu akisema kwamba mashabiki wa Shabana FC walistahili matokeo bora.
Shabana FC imerejea kwenye ligi kuu nchini Kenya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 17.