Serikali ya kaunti ya Nairobi leo Jumatano imefanya mkutano na miungano ya waendesha bodaboda wa katikati ya jiji la Nairobi.
Lengo la kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Green Park na kuongozwa na afisa mkuu wa usalama na mipangilio ya jiji Toni Kimani, lilikuwa kudumisha ushirikiano wa utendakazi baina yao.
Kwenye mkutano huo, iliafikiwa kuwa kila mwendesha bodaboda atavalia kiakishi kilicho na jina la muungano wake na nambari yake ya kazi kwa lengo la kutambuliwa miongoni mwao, wateja na maafisa wa usalama.
Kimani pia aliwahimiza kufanya kazi na kampuni mbalimbali hasa kwa kuvalia viakishi vya matangazo ya kampuni hizo.
Kampuni hizo zitawalipa, hivyo kuongeza mapato na kuboresha maisha yao.
Kupitia mkutano huo, waendeshaji bodaboda hao walishukuru uongozi wa Gavana Sakaja kwa kuwakubalia kuhudumu katikati ya jiji. Waliongeza kuwa watalipa ushuru na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za serikali ya kaunti hiyo.