Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, amewataka viongozi wanaume kupinga visa vya mauaji ya wanawake, akidokeza kuwa ongezeko la visa hivyo linaibua wasiwasi hapa nchini.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 73 ya kanisa la African Divine (ADC), Jijini Nairobi, Sakaja alielezea haja ya kuchukuliwa kwa hatua za haraka kuunga mkono mifumo inayowalinda wanawake dhidi ya dhuluma za kijinsia.
Kwa ushirikiano na mwakilishi mwanamke wa kaunti ya Nairobi Esther Passaris, Sakaja alitangaza mipango ya kubuni makao ya kuwalinda waathiriwa wa dhuluma za kijinsia katika eneo la Gigiri.
Makao hayo kulingana na Gavana huyo yatatumika kuwalinda wale ambao wanatoroka dhuluma za kijinsia na hivyo kupiga jeki juhudi za kitaifa za kushughulikia mauaji na dhuluma dhidi ya wanawake.
“Juzi tulipata mwili wa mwanamke umetupwa katika makaburi ya Lang’ata. Lilikuwa jambo la kusikitisha. lazima tuchukue hatua,” alisema Sakaja.
“Pamoja na Esther, tumejitolea kujenga jumba la kuwalinda waathiriwa wa dhuluma za kijinsia. Iwapo upo katika mazingira ambayo sio salama, usiendelee kukaa hapo kwa sababu yatagharimu maisha yako,” aliongeza Gavana huyo.
Aliwashutumu wanaotekeleza ghasia dhidi ya wanawake, akiwataka kukomesha vitendo hivyo mara moja.