Safaricom Chapa Dimba: Timu nne zafuzu kwa mashindano ya ukanda wa Rift Valley

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu nne zimejikatia tiketi kwa mashindano ya Safaricom Chapa Dimba, ukanda wa bonde la Ufa kufuatia kukamilika kwa mechi za mchujo wa wilaya.

Mabingwa watetezi wa ukanda huo Laiser Hill Academy kutoka kaunti ya Kajiado, Mwenge FC ya Nakuru, Trinity Mission Girls kutoka Nakuru na Ol Melil Girls ya Narok zilifuzu baada ya kushinda mechi za mchujo zilizoandaliwa katika kaunti za Bomet na Nakuru.

Timu hizo zinajiunga na nne zilizokuwa zimefuzu awali zikiwemo Wiyeta Girls, Itigo Girls, Ndura Sports, na PASC Langa FC na zitacheza mashindano ya ukanda yatakayoandaliwa wikendi hii katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Nakuru.

Katika mechi ya jana Jumapili katika uwanja wa chuo cha mafunzo cha Kisayansi na kiufundi cha Rift Valley, Mwenge FC ya Nakuru iliwacharaza Lorubae FC ya Samburu magoli manne kwa bila, ukiwa ushindi wa pili baada ya kuwakung’uta Mighty Lakers magoli 9 kwa sifuri.

Lorubae pia ilifuzu kwa fainali ya ukanda baada ya kuwabwaga Bamba Youth kutoka Baringo mabao 2-0.

Katika upande wa wasichana, Trinity Mission Girls ambao ni mabingwa wa Nakuru waliimenya Ridges Queens kutoka Nyandarua magoli 2-1 katika mchuano wa pili baada ya kuwalemea Kisima Girls ya Samburu 1 bila katika pambano la ufunguzi.

Website |  + posts
Share This Article