Rais William Ruto amemlimbikizia sifa sufufu Prof. Kithure Kindiki baada ya kuapishwa kuwa Naibu Rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya chini ya katiba mpya ya mwaka 2010.
Akihutubu katika ukumbi wa KICC punde baada ya Prof. Kindiki kula kiapo cha utenda kazi, Ruto amesema Prof. Kindiki ana tajriba pana ya kuipeleka Kenya mbele kwani ni mchapakazi mwenye bidii.
Ruto amemtaka Prof. Kindiki kudumisha kiapo cha utenda kazi na kiapo cha uaminifu bila uoga wala mapendeleo.
Nyakati zingine akumuita Abra K, ufupisho wa Abraham Kindiki, Ruto amemtaka Naibu wake mpya kuweka maslahi ya Wakenya wote mbele kwenye majukumu yake.
Rais amewataka Magavana, wabunge na wawakilishi wadi kuwatumikia Wakenya wote kwa uadilifu bila kujali ikiwa waliwapigia kura au la.
Rais ameelezea tukio la kihistoria la uapisho wa Prof. Kindiki kuwa ishara ya ukomavu wa asasi za Kenya.