Ruto: Waliofuja fedha za ufadhili wa masomo Uasin Gishu wazirejeshe la sivyo…

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto

Yeyote aliyefuja fuja fedha za mpango wa ufadhili wa masomo ya wanafunzi kutoka kaunti ya Uasin Gishu katika nchi za Canada na Ufini lazima wazirejesha la sivyo wakione cha mtema kuni. 

Rais William Ruto, wakati akivunja kimya chake kuhusu sakata hiyo ameahidi kutafuta njia za kuwasaidia wanafunzi walioathirika chini ya mpango huo kwa kuwafadhili kusomea humu nchini punde uchunguzi utakapokamilika.

Wazazi wanasemekana kupoteza zaidi ya shilingi milioni 800 walizotoa kufadhili masomo ya wanao katika nchi za Canada na Ufini chini ya mpango huo.

“Mambo ya uchunguzi inaendelea. Kama kuna mtu alikula hiyo pesa ajipange kulipa ama aingie taabani. Hakuna kubembelezana,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia wakazi wa mji wa Eldoret leo Jumatano.

“Mara tu uchunguzi utakapokamilika, tutaona namna ya kuwasaidia wanafunzi walioathirika kwa kuwapa ufadhili ili wasomee humu nchini na kutimiza ndoto zao.”

Aliyasema hayo wakati Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imeagiza kukamatwa kwa Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu  Jackson Mandago na watu wengine watatu kuhusiana na sakata hiyo.

Watatu hao ni Joseph Kipkemoi Maritim, Meshak Rono na Joshua Kipkemoi Lelei.

Wanatarajiwa kukabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutumia vibaya mamlaka na kufanya njama ya kuiba.

Washukiwa wanatuhumiwa kwa kufanya njama ya kuiba shilingi bilioni 1 kutoka kwenye akaunti iliyopo kwenye benki ya KCB iliyosajiliwa chini ya Hazina ya Uasin Gishu.

Fedha zilizowekwa kwenye akaunti hiyo zilikusudiwa kulipa karo ya wanafunzi kutoka kwenye kaunti hiyo chini ya mpango wa masomo nje ya nchi wa kaunti ya Uasin Gishu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *