Ruto: Walimu 20,000 kuajiriwa kufikia mwezi Januari 2025

Martin Mwanje
2 Min Read

Serikali ina mipango ya kuwaajiri walimu 20,000 zaidi kufikia mwezi Januari mwakani. 

Rais William Ruto anasema hatua hiyo inalenga kuangazia changamoto zinazoikumba sekta ya elimu hususan tangu kuasisiwa kwa mfumo wa mtaala wa umilisi, CBC.

Rais Ruto amesema serikali ya Kenya Kwanza anayoiongoza tayari imewaajiri walimu 56,000 hadi kufikia sasa katika juhudi za kupiga dafrau baadhi ya changamoto hizo.

“Pia tumehakikisha mpito mzuri wa wanafunzi kutoka shule ya msingi hadi sekondari ya msingi, JSS na kuziweka Gredi za 7,8 na 9 katika shule za msingi, kwa kutumia ipasavyo miundombinu iliyopo, kuhakikisha usalama wa wanafunzi vijana na kuwalinda wazazi dhidi ya gharama kubwa zinazohusiana na shule za malazi,” amesema Rais Ruto wakati akilihutubia taifa kutoka Bunge la Taifa.

Kulingana na Ruto, sekta ya elimu ilikabiliwa na janga kufikia mwaka 2022 huku ikiwa haijabainika namna mpito kuelekea CBC utakavyofanywa.

Ameongeza kuwa kufikia wakati huo, kulikuwa na uhaba wa walimu 11,000 na vyuo vikuu vya umma 23 kati ya 40 vilikaribia kufilisika na kukabiriwa na hatari ya kufungwa.

Miongoni mwa vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Nairobi, kile cha Kenyatta, Moi, Egerton, Maseno na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.

Hata hivyo, Rais anasema mfumo mpya wa ufadhili wa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ulioanzishwa na serikali yake umebadili mambo katika vyuo vikuu na kuviepushia hatari ya kufungwa.

 

 

 

Share This Article