Ruto: Tumeweka sera za kubadilisha Kaskazini mwa Kenya

Rais aliyasema hayo alipokutana na viongozi wa eneo la Kaskazini mwa nchi katika Ikulu ya Nairobi.

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto alipokutana na viongozi wa Kaskazini mwa Kenya katika Ikulu ya Nairobi

Serikali ya Kenya Kwanza inafanya kazi na viongozi wa eneo la Kaskazini mwa nchi kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakumba wakazi wa eneo hilo. 

Rais William Ruto amesema ushirikiano huo ni mojawapo wa jitihada za kuharakisha utekelezaji wa maendeleo katika eneo hilo lililotengwa kwa muda mrefu.

“Sera zetu za kimakusudi zinakomesha kutengwa kwa miongo kadhaa kwa kuhakikisha ustawi wenye usawa, upanuaji wa huduma muhimu na kubuni fursa zaidi za kiuchumi,” alisema Rais Ruto wakati alipokutana na viongozi kutoka eneo la Kaskazini mwa nchi katika Ikulu ya Nairobi.

“Mipango ya kimkakati kama vile Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu ulioanzishwa siku chache zilizopita itatoa rasilimali zinazohitajika kuwekeza katika uzalishaji wa nishati, ukusanyaji na uhifadhi wa maji, na unyunyiziaji mashamba maji ili kufungua uwezo wa kiviwanda na kilimo wa eneo hilo.”

Viongozi waliohudhuria mkutano huo walitoka kaunti za Isiolo, Marsabit, Garissa, Wajir na Mandera.

Waliongozwa na Waziri wa Afya Aden Duale na Magavana Ahmed Abdullahi (Wajir), Nathif Jama (Garissa) na Mohamed Khalif  wa Mandera.

Share This Article