Ruto: Shirikisho la Kisiasa ni muhimu kwa utangamano wa EAC

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto amesema maono ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni safari isiyokuwa ya kawaida kuelekea utangamano wa kina wa jumuiya hiyo. 

“Ingawa kuna changamoto ambazo lazima tuzishinde, manufaa yanayoweza kufikiwa kutokana na shirikisho kama hilo ni mengi,” alisema Rais Ruto wakati wa Tukio la Pembezoni la Ngazi za Juu la Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa EAC lililofanyika mjini Arusha nchini Tanzania leo Ijumaa.

“Kenya inaahidi kuendelea kutekeleza wajibu wake katika kuongoza safari hii kupitia ushirikishanaji wa tajiriba, kufikia makubaliano, msaada wa fedha na kuhakikisha kuna mazingira mwafaka ya umoja wa EAC.”

Rais William Ruto aliwasili mjini Arusha leo Ijumaa kuhudhuria Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo unatarajiwa kuangazia mpango wa ufadhili endelevu wa nchi nane wanachama wa jumuiya hiyo.

Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki pia itajadiliwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili.

Ruto amejumuika na Marais wenzake Samia Suluhu wa Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, Salva Kiir (Sudan Kusini ambaye ni mwenyekiti anayeondoka wa jumuiya hiyo), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Evariste Ndayishimiye (Burundi), Felix Tshisekedi (DRC) na Hassan Sheikh (Somalia).

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa tena kwa EAC pia yanaandaliwa.

“Tunapaswa kutumia ipasavyo fursa zinazoibuka na kujenga EAC ambayo ni thabiti zaidi na yenye ushindani abayo itaharakisha kuanzishwa kwa soko moja la Afrika,” amesema Ruto.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *