Rais William Ruto amesema serikali itaendelea na mpango wake wa kuwachanja mifugo uliopangwa kutekelezwa mwezi Januari mwakani.
Mifugo wanaolengwa kuchanjwa kwenye mpango huo ni ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50.
“Tunawaunga mkono wakulima katika kudumisha hatua zilizopigwa katika uzalishaji wa kilimo, ambazo zimeongeza mapato yao na kuboresha usalama wetu wa chakula,” amesema Rais Ruto.
“Ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kikamilifu kutokana na fursa za kimataifa, tutatekeleza mpango mpana wa utoaji chanjo, kwa kutumia chanjo zilizozalishwa humu nchini, ili kupunguza kuenea kwa maradhi kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.”
Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumanne wakati wa Tamasha la Kitamaduni la Baringo na Mnada wa Mbuzi wa Kimalel.
Matamshi yake yanakuja wiki moja baada ya kiongozi huyo wa nchi kuwapuuzilia mbali baadhi ya viongozi wa upinzani wanaopinga mpango wa kutoa chanjo kwa mifugo kote nchini akisema utasaidia kuimarisha afya ya mifugo na uwezo wa kuuza nyama nje ya nchi.
Kulingana naye, mpango huo, unaolenga kuwachanja ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50, unalenga kukabiliana na maradhi ya kuvuka mpaka kama vile ugonjwa wa miguu na midomo.
“Wale wanaopinga mpango huo hawana sababu na labda hawana ng’ombe. Wakati tunapokuwa na mazungumzo kuhusu ng’ombe, fyata tu ulimi ikiwa hauna ng’ombe,” alisema Rais Ruto wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la 4 la Uongozi la Wafugaji katika kaunti ya Wajir wiki moja iliyopita.
Aliongeza kuwa chanjo itakayotumiwa ni ile inayozalishwa na Taasisi ya Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo nchini Kenya (KEVEVAPI) na ambayo huzalisha chanjo za mifugo ambazo ni salama kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi nchini.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa mstari wa mbele kupinga mpango wa kuwachanja mifugo mwezi Januari mwakani akitilia shaka usalama wa chanjo itakayotumika.