Kila Waziri atawajibikia utendakazi wa wizara yake ifikapo kila mwisho wa mwaka wa fedha.
Rais William Ruto amesema anaratajia kila Waziri kuchukua jukumu la kibinafsi katika kufikia malengo yaliyoelezwa katika kandarasi za utendakazi za wizara zao.
“Mwishoni mwa mwaka wa fedha, kila Waziri atapokea ripoti ya utendakazi inayoakisi mafanikio ya wizara zao. Ripoti hizi zitahakikisha kandarasi za utendakazi hazionekani kama tukio lisilokuwa na maana,” alisema Ruto wakati wa hafla ya utiaji saini wa kandarasi za utendakazi za wizara za mwaka wa fedha 2024/2025 iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.
“Kandarasi hizi zitatumiwa kwa ajili ya utambuzi, kutoa tuzo au vikwazo, ambavyo vitatolewa bila kukosa. Ubora, uadilifu, utendakazi mzuri na uendelevu utatuzwa huku kushindwa kutimizwa ahadi hizo, utepetevu, matumizi mabaya ya rasilimali na mienendo mibaya ikichochea hatua sahihishi.”
Rais Ruto aliwataka mawaziri hao kufanya kila wawezalo kutimiza ahadi zilizotolewa na serikali ya Kenya Kwanza kwa Wakenya akiongeza kuwa anawategemea kumsaidia kutimiza ahadi hizo.
“Tunaposaini kandarasi za utendakazi za wizara za kizazi cha pili za mwaka wa fedha wa 2024/2025, hebu tuakisi ahadi tulizotoa na uzito wa wajibu wetu,” aliongeza Ruto.