Ruto: Mageuzi katika idara ya polisi yataendelea ilivyokusudiwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akipokea ripoti juu ya mageuzi ya polisi katika Ikulu ya Nairobi

Rais William Ruto amesema serikali imekusudia kufanya mageuzi makubwa yatakayohakikisha idara ya polisi inatiwa motisha, ina rasilimali za kutosha na inafanya kazi kitaaluma. 

Ruto amesema kuna hatua zilizodhihirika kupigwa katika kuhakikisha idara hiyo inapata vifaa vya kisasa vya utendakazi.

“Tunataka kuhakikisha kuwa maafisa wa polisi wanaohahatarisha maisha yao wanapokuwa kazini wana vifaa vya kujikinga, na wanaungwa mkono na serikali,” alisema Rais Ruto wakati akipokea ripoti ya mwisho wa muhula ya Tume ya pili ya Taifa ya Polisi  katika Ikulu ya Nairobi.

Tume hiyo iliteuliwa mwezi Machi mwaka 2019 kwa kipindi kisichoweza kuongezwa cha miaka sita.

Wanachama wa tume hiyo walikuwa Eliud Kinuthia ambaye alihudumu kama Mwenyekiti, Dkt. Alice Otwala ambaye alihudumu kama Naibu Mwenyekiti, John Ole Moyaki, Eusebius Laibuta, Dkt. Lilian Kiamba na Edwin Chelugut.

Rais aliipoongeza tume hiyo kwa mchango wao kwa mageuzi ya polisi na usimamizi wa wafanyakazi wa idara ya polisi.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen ni miongoni mwa waliokuwapo wakati wa kupokea ripoti hiyo.

Mafanikio makuu ya Tume ya pili ya Huduma ya Taifa ya Polisi ni pamoja na kuajiriwa kwa maafisa wa polisi 10,982 na wafanyakazi raia 1,128.

Aidha, tume hiyo ilisimamia upandishaji vyeo wa maafisa wa polisi 16,000, uhamishaji wa maafisa 26,000, utoaji nidhamu kwa maafisa 1,400 na kushughulikia rufaa 700.

 

Website |  + posts
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *