Ruto: Mabadiliko katika sekta ya kahawa yanazaa matunda

Martin Mwanje
1 Min Read

Mabadiliko yanayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza katika sekta ya kahawa yameanza kuzaa matunda. 

Rais William Ruto anasema mabadiliko hayo yamehakikisha mkulima wa zao hilo hivi karibuni watapata mara nne ya malipo yao ya advansi kutokana na zao hilo.

Anasema malipo hayo yameongezwa kutoka shilingi 20 kwa kila kilo moja ya kahawa hadi shilingi 80 kutokana na kutengwa kwa shilingi bilioni nne kutoka kwenye Hazina ya Kahawa.

“Kanuni za mabadiliko yanayofanywa katika sekta ya kahawa zitawapatia wakulima uwakilishi unahitajika na usemi katika soko la mnada la Nairobi,” alisema Rais Ruto katika hotuba yake kwa taifa katika majengo ya bunge.

“Hatua hizi zinatarajiwa kusaidia juhudi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na kupanua uzalishaji hadi kaunti mpya na kuongeza maradufu uzalishaji wa kahawa katika kipindi cha miaka minne ijayo.”

Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa mstari wa mbele kupigia debe zao la kahawa na amekuwa akifanya juhudi za kupanua soko la zao hilo katika mataifa ya ughaibuni.

Wiki chache zilizopita, aliandamana na baadhi ya wakulima wa zao hilo hadi nchini Colombia kulinadi zao hilo.

Naibu Rais amekuwa akisisitiza kuwa wakati umewadia wa kuhakikisha kuwa madalali katika sekta ya kahawa wanaangamizwa kwa manufaa ya mkulima.

Share This Article