Rais William Ruto amesema mabadiliko katika mfumo wa kimataifa wa fedha yatasaidia kuongeza imani ya uwekezaji barani Afrika.
Rais Ruto amesema kuichukulia Afrika kama bara lisilokuwa hatari itasaidia kuboresha uhusiano kati ya sekta ya umma na ile ya binafsi kwa manufaa ya wote.
Amesema mfumo wa sasa wa fedha ambao umezichukulia kimakosa nchi zinazostawi kama mahali hatari pa kuwekeza umekuwa kikwazo kwa bara hilo.
“Hakuna namna unavyoweza kupata fedha za sekta ya binafsi barani Afrika usipoangazia suala la hatari. Hakuna atakayewekeza hapa,” alisema Rais Ruto.
Alitoa kauli hizo wakati wa Mazungumzo ya Rais ya Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) yenye kichwa “Kenya: nguvu inayoharakisha Biashara na Uwekezaji barani Afrika”, kaunti ya Nairobi.
Waliokuwapo ni pamoja na Katibu Mkuu wa UNCTAD Rebeca Grynspan, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi na Mawaziri Moses Kuria wa Biashara na Njuguna Ndung’u wa Fedha.
Kulingana na Rais, upatikanaji ulioongezeka wa fedha za maendeleo utaisaidia Afrika kuboresha miundombinu, kuongeza ushirikiano na kuchochea biashara baina ya mabara.
Alitoa wito wa uwezeshaji na taratibu za forodha kupigwa msasa ili kuimarisha biashara barani Afrika.
“Tunapaswa kuondoa vikwazo visivyokuwa vya ushuru wa forodha, kurahisisha utoaji nyaraka na kuwezesha kusogea kwa biashara na watu mipakani,” aliongeza Ruto.
Alisema Afrika inapaswa kuchukua hatua madhubuti kudai mgao wake kwa usawa katika biashara ya kimataifa, akiongeza kuwa asilimia 3 ya sasa haiendani na idadi ya watu walio barani humo.