Ruto: Kenya kuwa na uwanja mpya wa ndege miezi 18 ijayo

Ujenzi wa JKIA unakusudia kupanua uwezo wake, kuimarisha usalama na huduma za kushughulikia mizigo pamoja na abiria, pamoja na kuboresha nafasi ya Kenya kama kitovu cha safari za ndege katika kanda hii.

Martin Mwanje
2 Min Read

Ujenzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA unaendelea kwa leng0 la kuifanya Kenya kuwa kituo kinara cha kibiashara barani Afrika. 

Hususan, ujenzi huo unakusudia kupanua uwezo wa JKIA, kuimarisha usalama na huduma za kushughulikia mizigo pamoja na abiria, pamoja na kuboresha nafasi ya Kenya kama kitovu cha safari za ndege katika kanda hii.

Rais William Ruto anasema ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 18 ijayo.

“Kwa sasa ujenzi unaendelea katika uwanja huo wa ndege. Katika kipindi cha miezi 18, tutakuwa na uwanja mpya wa ndege,” alisema Rais William Ruto wakati akihutubia kongamano la kibiashara katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC jijini Nairobi leo Jumatano.

“Tutakamilisha ujenzi wa uwanja huo, kwa sababu hatuna uwanja wa ndege. Kwa wale mnaosafiri, unapowasili JKIA, unakutana na lami na uwanja huo hauko katika hali nzuri. Hivyo tutabadilisha hilo, katika kipindi cha miezi 18 ijayo tutakuwa na uwanja mpya wa ndege.”

Mnamo mwezi Juni mwaka huu, serikali ya Kenya ilitia saini kandarasi yenye kima cha shilingi bilioni 154.2 na kampuni ya ujenzi wa barabara na madaraja (CRBC) ya China ili kupanua uwanja wa JKIA.

Kandarasi hiyo ilitiwa saini na Katibu wa Safari za Ndege na Uendelezaji wa Anga Teresia Mbaika kwa niaba ya serikali ya Kenya, huku kampuni ya CRBC ikiwakilishwa na Meneja Mkuu Yu Xiaodong.

Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, kupitia ukurasa wake wa X, alisema mchakato wa utoaji zabuni hiyo ulitekelezwa kwa muda wa miezi mitatu, baada ya kukamilika kwa ramani ya JKIA mwezi Februari mwaka huu.

Zaidi ya kampuni 40 zilishiriki kwenye kongamano la kabla ya kutuma maombi ya zabuni lililoandaliwa mwezi Aprili mwaka 2026, ambalo lilifafanua matarajio ya mradi huo.

 

 

 

Share This Article