Ruto apigia debe ushirikiano wa kimkakati kati ya Kenya na Korea Kusini

Kevin Karunjira
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumanne alihutubia Kongamano la kwanza la Korea Kusini na Afrika na kusisitiza wajibu muhimu ambao Korea Kusini inaweza ikatekeleza katika kuleta mabadiliko barani Afrika. 

Ruto alisema bara la Afrika iko na shauku ya kutafuta ushirikiano thabiti na wawekezaji wa Korea Kusini ili kubadilisha uwezo mkubwa wa bara hilo kuwa fursa na uwekezaji ambao utabuni ajira na kuchochea ukuaji uchumi.

Aliongeza kuwa mali za Afrika, wakiwemo vijana wenye ujuzi, ardhi ya kutosha ya kilimo, hifadhi kubwa za nishati mbadala na na rasilimali nyingi za madini bado hazijatumiwa kikamilifu.

Kulingana na Ruto, Afrika imetambua usalama wa chakula, sayansi na teknolojia, amani na usalama na usalama wa afya kuwa nyanja muhimu za ushirikiano na Korea Kusini.

“Kongamano hili linaonyesha azimio la kuimarisha uhusiano huu na kutumia utayari wa kisiasa unaohitajika kwa Afrika na Korea Kusini kustawi pamoja kupitia ushirikiano wenye manufaa ya pande mbili. Ili kufanya hili, ni lazima tutumie kukamilishana kwetu na kutekeleza mikakati inayonufaisha pande zote kwa msingi wa ushirikiano wenye usawa,” alisema Rais Ruto.

Kongamano hilo, ambalo kaulimbiu yake ni Mustakabali Tunaotengeneza Pamoja: Ukuaji wa pamoja, Uendelevu na Umoja, liliandaliwa na Rais Yoon Suk Yeol katika Kituo cha Maonyesho ya Kimataifa cha Korea mjini Goyang.

Share This Article