Rais William Ruto leo Jumatatu anaongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Nairobi ambapo suala la mafuriko linatarajiwa kupewa kipaumbele.
Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi wamewaongoza mawaziri katika kuhudhuria mkutano huo.
Ni mkutano unaoandaliwa wakati mvua za El Nino zinaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuwa chanzo cha mafuriko ambayo yamesababisha madhara si haba.
Watu zaidi ya 50 wameripotiwa kufariki, maelfu wameachwa bila makazi, barabara zimeharibiwa na madaraja kusombwa, hali ambayo imetatiza usafiri katika maeneo mengi.
Kaunti za Mombasa, Mandera, Isiolo na Wajir ni miongoni mwa zile zilizoathiriwa zaidi kutokana na mafuriko hayo.
Wakati hali ikiendelea kuwa mbaya zaidi, Baraza la Magavana limetoa wito kwa serikali ya kitaifa kutangaza mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa kuwa janga la kitaifa.
Serikali kuu na zile za kaunti zimekuwa zikilumbana kuhusiana na utoaji fedha za kukabiliana na mafuriko hayo.
Hata hivyo, serikali kuu imewataka magavana kutenga fedha kutoka kwa bajeti zao na kutumia fedha za dharura kukabiliana na athari za mafuriko hayo.
Waliopoteza makao kwa upande wao wanazililia serikali zote mbili kuingilia kati na kuwaondolea kero la mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini kwa sasa.
Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imewaonya Wakenya kujiandaa kwa mvua zaidi.