Ruto amuaga Balozi Meg Whitman anayeondoka wa Marekani

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto leo Jumanne amekutana na kumuaga  Balozi wa Marekani nchini Kenya anayeondoka Meg Whitman. 

Whitman alitangaza kujiuzulu kwake kama Balozi wa Marekani humu nchini Novemba 13 mwaka huu.

Kwa kipindi ambacho amehudumu kwenye wadhifa huo, Whitman amekuwa na uhusiano mzuri na utawala wa Kenya Kwanza.

Kiasi kwamba mnamo mwezi Mei mwaka huu, Balozi huyo alikuwa mstari wa mbele katika kupanga ziara ya kitaifa iliyofanikiwa ya Rais Ruto nchini Marekani.

Hatua ya Whitman kujiuzulu wadhifa huo ilikuja siku chache baada ya Donad Trump kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani ulioandaliwa Novemba 5.

“Leo (Novemba 13), naitangazia timu yangu kwenye Ubalozi wa Marekani kuwa niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Biden. Imekuwa ni heshima kuwahudumia watu wa Marekani kupitia kuimarisha ushirikiano wetu na Kenya,” alisema Whitman katika taarifa ya kujiuzulu kwake wakati huo.

“Najivunia kuongoza ajenda iliyojikita kwa watu ambayo inaokoa maisha, kuongeza usalama na kubuni nafasi za kiuchumi kwa Wakenya na Wamarekani.”

Whitman alitaja utoaji wa fedha za dharura kukabiliana na mafuriko ya mwaka 2023, mapambano yanayoendelea dhidi ya ugonjwa wa malaria, Ukimwi na Mpox kuwa ushahidi tosha kuwa Marekani inatoa kipaumbele kwa afya na ustawi wa Kenya.

Hususan, Balozi huyo anayeondoka alitaja hatua yake ya kujiuzulu kuwa iliyotokana na uchaguzi wa urais uliofanyika nchini mwake siku chache zilizopita.

“Kama mabalozi wote wa Marekani, nahudumu kufuatia ombi la Rais. Watu wa Marekani wamezungumza na Rais mpya ataapishwa mwezi Januari. Namtakia yeye na timu yake mpya mafanikio,” alisema Whitman katika taarifa iliyoelezea baadhi ya mafanikio yake wakati wa kipindi chake cha kuhudumu.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump ataapishwa Januari 20 mwakani, na ilikuwa wazi kwamba angemteua Balozi mwingine kuchukua nafasi ya Whitman kutokana na mirengo tofauti ya kisiasa wanayoegemea.

Whitman aliteuliwa kuhudumu kama Balozi wa Marekani nchini Kenya na Rais Joe Biden wa chama cha Democrat wakati Trump ni wa kutoka chama cha Conservative kilichovuna ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Novemba 5.

Website |  + posts
Share This Article