Rais William Ruto amempongeza Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kwa kuibuka mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo siku chache zilizopita.
Aidha, Ruto amewapongeza raia wa nchi hiyo kwa mara nyingine kuudhihirishia ulimwengu kuwa India imekomaa kidemokrasia.
“Wakati ukisonga mbele, Mheshimiwa Modi, nina imani kuwa kujitolea kwako katika kuboresha India kutaongeza kasi ya ukuaji na maendeleo, na hivyo kuimarisha umoja na ustawi wa taifa,” alisema Ruto kupitia mtandao wake wa X.
Alielezea kujitolea kwa Kenya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Modi ametangaza kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo kwa wiki kadhaa.
Uchaguzi huo ulianza mwezi Aprili mwaka huu huku kukiwa na viti 543 vya kushindaniwa katika Baraza la Chini la Bunge la India.
Ingawa muungano unaoongozwa na chama tawala umeendelea kuwa na viti vingi, chama cha Modi cha Bharatiya Janata, BJP kilishindwa kupata wingi wa viti wa chama kimoja.
Shughuli ya kuhesabu kura ilianza jana Jumanne.
Matokeo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi mapema leo Jumatano yalionyesha kwamba muungano wa Modi unaoongozwa na BJP ulipata viti 293.
Kutokana na matokeo hayo, muungano huo huenda ukaharakisha mazungumzo kwa nia ya kuendeleza utawala wa Modi kwa muhula wa tatu. Idadi ya viti ambavyo chama cha BJP kilipata ilipungua hadi 240.
Wachambuzi wanasema upunguaji huo unatokana na hali ya wapiga kura kutoridhishwa na tofauti za kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ajira unaoongezeka nchini humo.