Ruto akutana na viongozi wa Ukambani, asisitiza umuhimu wa ushirikiano

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wakati wa mkutano na viongozi wa Ukambani katika Ikulu ya Nairobi

Ilikuwa ni zamu ya viongozi wa Ukambani kuzuru Ikulu ya Nairobi na kukutana na Rais William Ruto ili kuelezea matamanio yao ya maendeleo kwa kiongozi wa nchi. 

Viongozi waliokutana na Rais Ruto leo Alhamisi walikuwa wa kutoka kaunti tatu za Ukambani za Machakos, Kitui na Makueni.

Ziara yao inakuja siku moja baada ya Rais Ruto kukutana na viongozi kutoka eneo la magharibi katika Ikulu iyo hiyo.

Wakati wa mkutano wa hii leo, Rais Ruto alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka kando tofauti zao na kuwahudumia Wakenya ipasavyo.

“Tunapaswa kukumbatia uongozi wa ushirikiano, hata tukiwa na miegemeo yetu inayokinzana ya kisiasa, ili kuiunganisha na kuibadilisha Kenya,” alisihi Rais Ruto.

“Kupitia kufanya kazi kama timu, tutaharakisha utoaji huduma na maendeleo ya nchi yetu.”

Rais Ruto anaonekana kuanza kupanua wigo wa uungwaji mkono wake wakati mirindimo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ikianza kusikika kwa mbali.

Eneo la Ukambani inachukuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, na wachanganuzi wa mambo wanasema Ruto analenga kuwatumia viongozi hao kujinadi kwa jamii ya Wakamba.

Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua amekuwa mstari wa mbele kuwashawishi wakazi wa Ukambani kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza ili kufaidika kwa kiwango kikubwa na miradi ya maendeleo.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *