Rais William Ruto amekagua na kuanzisha miradi kadhaa ya maendeleo katika eneo bunge la Emurua Dikirr, kaunti ya Narok.
Katika ziara yake siku ya Jumatano, Rais Ruto amekagua ujenzi wa soko la kisasa la Mamboleo ambalo litaselehi wafanyabiashara 250 punde litakapokamilika.

Baadaye, Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu cha Trans Mara East KMTC alikowahutubia wananchi.
Ruto ameahidi kuwa serikali itatekeleza miradi ya maendeleo kila sehemu ya nchi bila kujali miegemeo ya kisiasa.
Amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali ya nchi na kuzindua miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, masoko ya kisasa, hospitali na kadhalika.
Kabla ya kuelekea Narok, Ruto alitembelea kaunti ya Taita Taveta alikozindua miradi kadhaa ya maendeleo.
Upinzani unamtuhumu kwa kutumia miradi hiyo kama chambo cha kuwavutia wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.