Rais William Ruto ametoa wito kwa kampuni za Kijapani kuwekeza katika sekta za utengenezaji bidhaa, kilimo na teknolojia nchini Kenya.
Amesema utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi Kuanzia Chini hadi Juu ya serikali imefungua fursa nyingi katika sekta hizo.
Aliongeza kuwa ushirikiano huo utasababisha matokeo yatakayofaidi pande zote mbili huku kampuni za Japani zikipata wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu kutoka Kenya wanaotafuta nafasi za ajira.
Rais Ruto alisema Kenya inaelekea kuwa kituo cha nguvukazi cha bara la Afrika ikiwa na wafanyakazi wenye umri wa miaka 20 walio na ujuzi, utaalam na werevu.
”Tunataka ubobezi wenu katika utengenezaji bidhaa nchini Kenya ili mzalishe bidhaa nchini humo na mtumie nguvukazi yetu yenye ujuzi wa hali ya juu. Hii itabuni nafasi za ajira kwa ajili ya vijana wetu,” alisema.
Rais Ruto aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa kongamano la biashara kati ya Kenya na Japani lililofanyika jijini Tokyo.
Alielezea kuwa kwa kuwekeza nchini Kenya, kampuni za Japani siyo tu kwamba zitafikia soko la Kenya, lakini pia Jumuiya ya Afrika Mashariki na soko la bilioni 1.4 la Afrika lililowezeshwa na makubaliano ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika, AfCFTA.
Kadhalika, Ruto aliwataka wawekezaji Wajapani kutumia ardhi ya kilimo ya Kenya aliyosema ina uwezo wa kutoa mchango mkubwa kwa usalama wa chakula duniani.
“Afrika, ikiwemo Kenya, ina ardhi ya kutosha ya kilimo kuzalisha chakula cha kukidhi mahitaji ya idadi ya watu wanaoongezeka duniani,” aliongeza Rais.