Rais Ruto aendelea kueneza injili ya nyumba za bei nafuu

Martin Mwanje
2 Min Read

Mpango wa nyumba za bei nafuu unaotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza utasaidia kupanua fursa za kiuchumi zitakazowanufaisha vijana humu nchini. 

Kadhalika, Rais William Ruto anasema mpango huo utasaidia kupunguza hulka ya kugawa mashamba ya kilimo katika vipande vidogo vidogo.

“Tunatumai kusimamisha hulka hii ili chakula kingi kiweze kuzalishwa kutoka kwenye mashamba yetu,” alisema Rais Ruto wakati akikagua ardhi iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu mjini Kitale.

Alisema mpango huo utatoa ajira kwa vijana wasiopungua 2,000 katika kaunti ya Trans Nzoa.

Katika siku za hivi karibuni, Rais Ruto amesisitiza kuwa hakuna chochote kitakachozuia utekelezaji wa miradi ya serikali na ametoa onyo kali kwa idara ya mahakama, akiitaka kukoma kushirikiana na watu fulani kuhujumu utekelezaji wa miradi hiyo.

Ameilaumu mahakama kwa kutoa maagizo ya usitishaji wa miradi hiyo mara kwa mara, maagizo anayosema yanatokana na ufisadi uliokithiri katika idara ya mahakama.

Idara ya mahakama ikiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome imetoa wito kwa kiongozi wa nchi kudhihirisha madai yake, na imeelezea nia ya kukutana naye kuzungumzia suala hilo.

Upinzani na chama cha mawakili, LSK ni baadhi ya wanaopinga mkutano kati ya Rais Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome.

Wanasema kufanyika kwa mkutano kama huo kutaathiri utendakazi wa idara ya mahakama.

Share This Article