Ruto aelekea magharibi mwa nchi, azindua miradi ya maendeleo

Martin Mwanje & PCS
2 Min Read
Rais William Ruto wakati akizindua hospitali ya Butere Level IV

Rais William Ruto Oktoba 30 alianza ziara ya maendeleo ya siku nne magharibi mwa nchi, siku chache baada ya kufanya ziara kama hiyo katika kaunti ya Nakuru.

Aliandamana na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na viongozi wengine wengi wa eneo hilo.

Ruto alianzia ziara yake katika eneo la Butere, alikozindua rasmi hospitali ya Butere Level IV, hospitali ya kisasa inayotarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ruto aliahidi kutoa shilingi milioni 150 zitakazotumiwa kununua vifaa tiba vitakavyowekwa katika hospitali hiyo.

Pia aliahidi kutoa shilingi zingine bilioni 1 zitakazotumika kukamilisha ujenzi uliokwama wa hospitali ya Kakamega County Level VI.

Ameitaja hospitali hiyo kuwa itakayobadilisha sekta ya afya kanda hiyo.

Akizungumza akiwa Butere, Ruto alielezea mipango mbalimbali ya maendeleo katika kaunti ya Kakamega, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa shilingi bilioni 2.2 wa uunganishaji wa umeme kwa hadi kaya 34,000, shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ukamilishaji wa uwekaji lami unaoendelea kwa barabara za eneo hilo na shilingi bilioni 1.4 zitakazotumika kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Bukhungu.

SpikaWetang’ula aliisifia serikali kutokana na miradi hiyo na kuwataka viongozi wa magharibi kuunga mkono juhudi za Rais Ruto kuongezewa muhula wa pili ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilishwa.

Wengine waliokuwepo ni Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, mtangulizi wake ambaye pia ni Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli miongoni mwa viongozi wengine.

Rais Ruto anatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali ya eneo la magharibi akizindua miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya barabara, afya na nishati.

Martin Mwanje & PCS
+ posts
Share This Article