Rais William Ruto amesema serikali inapanga kuhakikisha kila mwanafunzi atakayekubaliwa katika chuo kikuu, chuo cha ufundi au Taasisi ya Mafunzo ya Utabibu Nchini, KMTC anapata ufadhili kamili wa masomo.
Kiongozi wa nchi alikuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani, leo katika ukumbi wa michezo wa Kasarani Nairobi.
Alisema Mswada unaopendekezwa wa Elimu ya Juu, Uwekaji na Ufadhili wa Wanafunzi wa 2026 utahakikisha upatikanaji wa elimu ya juu unategemea uwezo na azma ya mwanafunzi badala ya kipato cha wazazi.
Kulingana naye, hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi yanayolenga kujenga upya mfumo wa elimu nchini na kuandaa wafanyakazi wenye ujuzi unaohitajika.
Ruto alisema ufadhili wa elimu umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 526 miaka minne iliyopita hadi Shilingi Bilioni 784.5, hivyo kuifanya elimu kuwa sekta inayopokea mgao mkubwa zaidi katika bajeti ya kitaifa.
Alisema ufadhili wa vyuo vikuu umeongezeka kutoka Bilioni 44 mwaka 2022 hadi Bilioni 82 katika mwaka uliopita wa kifedha, kufuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Ufadhili Unaomlenga Mwanafunzi.
Rais alihusisha mageuzi ya elimu na azma ya Kenya ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa, akisema teknolojia inawapa Wakenya fursa za kuuza huduma za kitaalamu kimataifa.
Alihimiza walimu kutumia zana za kidijitali, kukuza udadisi na ubunifu, akisema watoto hawawezi kupata ujuzi wa kesho kwa kutumia mbinu za jana.
Ruto alisema msisitizo wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ni muhimu katika kuandaa wabunifu na wataalamu watakaosaidia kukuza uchumi.