Ruto aahidi kuipa Kenya barabara za ubora wa hali ya juu

Martin Mwanje & PCS
2 Min Read
Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine katika Ikulu ya Nakuru

Rais William Ruto amesisitiza dhamira yake ya kuipa Kenya barabara za ubora wa juu zaidi, ikiwa ni pamoja na barabara ya Rironi-Nakuru-Mau Summit ambayo ujenzi wake utazinduliwa hivi karibuni. 

Ruto amesema angezindua ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 230 mapema, lakini hakuridhishwa na usanifu wake, ambao haukuzingatia idadi inayoongezeka ya magari kwenye barabara hiyo kuu ya usafiri.

“Nilipaswa kuzindua ujenzi wa barabara hii mwezi jana. Lakini nilipogundua kuwa itakuwa tu ya pande mbili yenye leni mbili, ambayo itazidiwa tena na msongamano wa magari ndani ya miaka tisa, niliagiza isanifiwe upya,” alisema Rais Ruto leo Jumanne.

Aliyasema hayo alipokutana na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Nakuru katika Ikulu ya Nakuru.

Kutokana na hilo, barabara hiyo ilisanifiwa upya ili kuwa barabara ya pande mbili yenye leni nne kutoka Rironi hadi Naivasha, huku ile ya Naivasha hadi Nakuru ikiwa ya pande mbili yenye leni sita.

Sehemu za barabara ya Rironi-Mai Mahiu-Naivasha na Nakuru-Mau Summit zitakuwa na leni nne.

“Hizi ndizo aina ya barabara unazopata katika nchi zilizostawi; sasa tunazijenga hapa nyumbani,” alisema Ruto.

Aliongeza kuwa: “Mungu akijalia, tutasherehekea Sikukuu ya Madaraka mwaka 2027 hapa katika kaunti ya Nakuru, na tutaitumia barabara hiyo.”

Barabara hiyo inafadhiliwa na kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC) na Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) chini ya mpango wa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Rais Ruto ameelezea kuwa anahitaji kujenga zaidi ya kilomita 1,000 ya barabara za pande mbili na kilomita zingine 10,000 ikiwa Kenya itajiunga na ligi ya mataifa yaliyoendelea duniani.

Waliokuwepo ni pamoja na Gavana wa Nakuru Susan Kihika na Mawaziri Lee Kinyanjui wa Biashara na Alice Wahome wa Ardhi miongoni mwa viongozi wengine.

Martin Mwanje & PCS
+ posts
Share This Article