Bingwa mara mbili wa Chicago Marathon Ruth Chepng’etich na bingwa wa London Marathon mwaka 2022 Amos Kipruto, ni miongoni mwa wanariadha wa Kenya waliotoa ithibati ya kushiriki makala ya mwaka huu ya Chicago Marathon yatakayofanyika mwezi Oktoba.
Chepng’etich aliye na umri wa miaka 30 atalenga kutwaa ubingwa wa mbio hizo kwa mara ya tatu baada ya kuibuka bingwa mwaka 2021 na 2022, huku akijivunia muda wa kasi wa saa 2 dakika 16 na sekunde 18.
Wakenya wengine watakaoshiriki ni bingwa wa London Marathon mwaka 2021 Joyceline Jepkosgei, Irene Cheptai, Dorcas Tuitoek, Mary Ngugi na Stacy Ndiwa.
Mbio za wanaume zitashuhudia Kipruto ambaye pia ni mshindi wa nishani ya shaba ya Dunia mwaka 2019 akipambana na Vincent Kipkemoi aliyemaliza wa tatu Tokyo Marathon mwaka huu na John Korir.
Makala ya 46 ya Chicago Marathon yataandaliwa Oktoba 13 nchini Marekani.