Urusi imeahidi kulipiza kisasi baada ya kile inachokitaja kuwa mashambulizi ya makombora dhidi yake yaliyotekelezwa na Ukraine.
Ukraine inaripotiwa kutumia makombora ya masafa marefu iliyopatiwa na Marekani, huku Urusi ikisema kwamba ilidungua makombora hayo manane yaliyorushwa katika eneo la Belgorod.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema kwamba Januari 3, 2025, jaribio la mashambulizi ya makombora lilitekelezwa kutoka kwa himaya ya Ukraine katika eneo la Belgorod.
Ilifafanua kwamba makombora hayo yametengenezewa nchini Marekani.
“Matendo haya ya serikali ya Ukraine, yanayoungwa mkono na marafiki wa magharibi, yatalipizwa” ilisema Wizara hiyo.
Maafisa wa Ukraine hawajasema lolote kuhusu mashambulizi hayo.
Mfumo wa makombora ya kimkakati – ATACMS una uwezo wa kufika umbali wa kilomita 300 na uliundwa kwa mara ya kwanza miaka ya 1980.
Rais anayeondoka wa Marekani Joe Biden alikuwa ameidhinisha Ukraine itumie silaha hizo dhidi ya Urusi mwaka jana, hatua iliyokashifiwa vikali na Russia kama ambayo ingezidisha zaidi mzozo wa miaka kama mitatu.
Biden anatarajiwa kutangaza usaidizi zaidi wa kiulinzi kwa Ukraine katika muda wa siku chache zijazo, kulingana na msemaji wa ikulu ya Marekani John Kirby.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump alisema katika mahojiano mwezi uliopita kwamba anapinga Ukraine kutumia silaha hizo, akisema zinazidisha mgogoro.