Mwigizaji wa Nollywood Ruby Ojiakor amechapisha picha za kabla ya harusi yake na mume wake Moc Madu ya kanisani.
Ruby na Moc ambaye pia ni mwigizaji wa Nollywood walionekana wenye furaha kwenye picha hizo za kabla ya harusi ambapo walichagua dhana ya tenisi.
Chini ya picha hizo walizopigiwa kwenye uwanja wa tenisi wakiwa na sare kamili ya mchezo huo Ruby aliandika, “Nimepotelea kwenye kina kirefu cha mapenzi, Napata milele yangu. Kila mtazamo, kila tabasamu, kila sekunde na wewe ni ya kipekee.”
Moc naye alichapisha picha hizo hizo kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alielezea kwamba kwake mapenzi yanamaanisha tenisi ambayo alitumia awali kujiliwaza lakini sasa akiwa na Ruby amekamilika.
Harusi ya kanisani ya wapenzi hao wawili inatarajiwa kuandaliwa Jumamosi Mei 31, 2025 huko Asaba, jimbo la Delta nchini Nigeria.
Wamekuwa wakifanya mipango kwa muda sasa hasa baada ya kuandaa harusi yao ya kitamaduni Februari Mosi, 2025 ambapo Ruby alionekana mwenye furaha na mchangamfu kiasi cha kuzua minong’ono mitandaoni.
Kwenye video moja Ruby alionekana akivua viatu na kumpa mtu kibeti amshikie huku akicheza kwa nguvu karibu na mume wake kabla ya kupiga magoti mbele yake.
Nyingine ilimwonyesha akiwa amevaa kitamaduni akichezea nyimbo zilizokuwa zikipigwa na bendi, hatua iliyoshangaza wafuasi wake mitandaoni.
Inasubiriwa kuona jinsi wahusika wa tasnia ya filamu nchini Nigeria watajitokeza kwa hafla hiyo.
 
					 
				 
			
 
                                
                              
		 
		 
		 
		