Enzi ya Ruben Amorim kama kocha mpya wa Manchester United imeanza leo Jumatatu baada kocha huyo kutua nchini Uingereza.
Amorim aliteuliwa kumrithi Ten Hag kufuatia msururu wa matokeo mabaya tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi kuu ya Uingereza.
Kwa sasa, Man U inashikilia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa alama 15 huku Liverpool ikiwa kidedea kwa alama 28.
Mholanzi na mchezaji wa zamani wa mashetani hao wekundu Ruud van Nistelrooy amekuwa kaimu kocha wa timu hiyo tangu Ten Hag alipopigwa kalamu.
Amorim, mwenye umri wa miaka 39, amenukuliwa akisema anafahamu kibarua kigumu kinachomsubiri uwanjani Old Trafford akiongeza kuwa yuko tayari kukivalia njuga.
Kabla ya kuteuliwa kwake kuiongoza Man U, Amorim amekuwa akihudumu kama kocha wa timu ya Ureno ya Sporting Lisbon.