Timu za Ufaransa, Romania na Slovakia zilianza vyema makala ya 17 ya bara Uropa kufuatia ushindi wao dhidi ya Austria, Ukraine na Ubelgiji mtawalia.
Mchuano baina ya Ufaransa na Austria ulichezwa ugani Merkur Spiel na ulikuwa wenye kasi huku kila timu ikidhihirisha sababu ya uwepo wao kwenye mashindano hayo.
Hata hivyo, baada ya hodihodi kwa lango la mpinzani, mshambulizi matata na sajili mpya wa Real Madrid Kylian Mbappe, aliandaa mpira uliomkanganya beki wa Austria Maximilian Wöber na kusababisha yeye kujifunga mnamo dakika ya 38.
Ngarambe hiyo iliendelea kwa mashiko makubwa hadi Mbappe akajeruhiwa pua na kuondolewa uwanjani ingawa alirudi bila ruhusa ya mwamuzi na kuketi uwanjani. Jambo hilo lilisababisha alishwe kadi ya njano kisha akaondolewa uwanjani kwa ajili ya matibabu na kuwaacha wachezaji 10 wenza.
Mechi hiyo iliisha kwa bao moja. Kwa sasa, Ufaransa ni wa pili kundini D kwa alama tatu sawia na viongozi Uholanzi walio walaza Poland mabao mawili kwa moja. Poland wanashika nafasi ya tatu nayo Austria ni ya nne.
Kwenye kundi E, Romania wanaongoza kwa alama tatu sawia na Slovakia ila wana mabao matatu na moja mtawalia. Mabao hayo matatu dhidi ya Ukraine yalifungwa na Nicolae Stanciu, Răzvan Marin na Denis Drăguș dakika ya 29, 53 na 57 mtawalia ugani Allianz Arena.
Bao la Slovakia dhidi ya Ubelgiji lillitiwa kimiani na Ivan Schranz dakika ya saba. Katika mchezo huo, Ubelgiji kupitia kwa mshambulizi hatari wa klabu ya Roma Romeo Lukaku, ilitia wavuni magoli mawili ila yalikataliwa.
Leo Jumanne, mechi za kwanza za makundi zitamalizika. Türkiye na Georgia watacheza saa moja jioni alafu saa nne usiku, Christiano Ronaldo aiongoze Ureno kupambana na Czechia.