Rekodi zaanguka katika Kombe la Dunia

Jumla ya magoli 216 yamefungwa, yakiwemo 215 katika mechi za makundi.

Dismas Otuke
2 Min Read

Rekodi kadhaa zimevunjwa siku 18 tangu kuanza kwa ngarambe ya 23 ya Kombe la Dunia katika mataifa ya Canada, Marekani na Mexico.

Mechi 73 zimechezwa zikiwemo 72 katika hatua ya makundi na moja  ya raundi ya 32 bora.

Mashabiki waliofika katika viwanja 16 vilivyo katika miji 16 ya mataifa matatu yanayoandaa fainali za mwaka huu kufikia mechi ya raundi ya 32 bora kati ya Afrika Kusini na Canada, ni milioni 4.7.

Aidha, kati ya wachezaji 1,248 kutoka timu 48 zinazoshiriki kombe hilo, wachezaji 999 wamejumuishwa katika mechi kufikia sasa.

Jumla ya magoli 216 yamefungwa yakiwemo 215 katika mechi za makundi, idadi hiyo ikipita ile ya makala yote ya mwaka 2022 nchini Qatar, ambapo magoli 172 yalifungwa katika mechi zote 64.

Nahodha wa Argentina Lionel Messi pia ameingia kwenye kumbukumbu kuwa mwanandinga wa kwanza kufunga bao katika fainali saba mtawalia alizoshiriki, akiwa pia mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia yakiwa 19 hadli wa leo.

Messi pia ni mchezaji mkongwe zaidi kufunga mabao matatu katika mchuano mmoja (Hat trick) akiwa na umri wa miaka 38, akipita rekodi ya Christiano Ronaldo aliyefunga mabao matatu mwaka 2018 akiwa na umri wa miaka 33.

Mashabiki zaidi ya milioni 4.7 kutoka mataifa 210 ya pembe zote duniani wamehudhuria mechi uwanjani, ikipita rekodi ya juu ya awali ya mashabiki  milioni 3.5 waliohudhuria Kombe la Dunia mwaka 1994.

Share This Article