Rejeeni vituoni au mkione cha mtema kuni, Dr. Omollo awaonya maafisa wa utawala

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri wa Ulinzi Aden Duale akiwa na Katibu wa Usalama wa Taifa, Dr. Raymond Omollo.

Maafisa wa utawala wa serikali wanaoendesha shughuli zao nje ya vituo vyao vya utendaji kazi wanakabiliwa na hatari ya kupoteza ajira zao kwa sababu ya kupuuza majukumu yao na kuhatarisha usalama wa taifa.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dr. Raymond Omollo amewaamrisha maafisa wote wanaofanyia kazi nyumbani kurejea na kuchukua udhibiti wa vituo vyao huku serikali ikiimarisha vita dhidi ya ugaidi.

Dr. Omollo alisema maafisa hao wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya magaidi na makundi mengine yenye dhamira potovu.

Alionya kuwa watakaokaidi onyo hilo watapigwa kalamu mara moja.

“Ikiwa unafanya kazi kama afisa wa utawala wa serikali ya kitaifa, hakikisha uko kwenye kituo chako cha kufanyia kazi. Na ikiwa hauwezi ukawa kwenye kituo chako cha kufanyia kazi, basi ni wakati wa kufunganya virago na kwenda zako,” alisema Katibu Omollo.

Waliolengwa katika ujumbe huo ni pamoja na Makamishna wa Kaunti, Manaibu na Wasaidizi wao pamoja na Machifu na Manaibu wao.

Alionya kuwa maafisa watakaozembea kazini wataadhibiwa.

Alikuwa akizungumza mjini Garissa alipoambatana na Waziri wa Ulinzi Aden Duale wakati wa mkutano wa usalama ulioandaliwa mjini Masalani na kuwaleta pamoja viongozi wa eneo hilo, wazee na maafisa wa utawala kutoka kaunti ndogo za Ijara, Hulugho, Bodhai na Bura Mashariki.

Miongoni mwa kaunti zingine katika eneo la Kaskazini Mashariki, kaunti ya Garissa imekumbwa na msururu wa matishio ya mara kwa mara kutoka kwa wanamgambo wa Al-Shabaab wanaoendelea kurandaranda karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *