Ratiba ya safari za ndege za KQ kutatizwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Huku msimu wa krismasi unapokaribia, Shirika la ndege la Kenya Airways limetangaza kutatizwa kwa ratiba ya safari zake kutokana na uhaba wa vipuri. 

Shirika hilo ambalo ni mojawapo wa mashirika makubwa zaidi ya safari za ndege barani Afrika, limesema limelazimika kuegesha baadhi ya ndege zake na hali hiyo huenda ikadumu kwa muda wa wiki mbili zijazo.

Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Allan Kilavuka kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, alisikitikia changamoto inayoshuhudiwa katika usambazaji wa vipuri vya ndege.

“Kutokana na ongezeko la safari za ndege wakati huu wa msimu wa sherehe, tungependa kuwafahamisha habari muhimu. Ratiba ya safari zitatatiza katika wiki kadhaa zijazo kutokana na changamoto zinazoshuhudiwa katika usambazaji wa vipuri vya ndege,” alisema Kilavuka.

Hatua hiyo imeathiri pakubwa mipango ya safari za abiria ambao wameshauriwa kuangalia mtandao au afisa wa uhusiano mwema wa shirika hilo kuhusu mabadiliko ya safari za ndege.

“Tunafahamu athari zilizopo kutokana na mabadiliko hayo, na tunaomba msamaha kuhusiana na hali hiyo. Tunafanya kila tuwezalo kupunguza athari hizo,” aliongeza Kilavuka.

“Tunatarajia hali hii itadumu kwa muda wa wiki mbili na tunawashukuru kwa kuwa watulivu, huku tukijizatiti kusuluhisha hali hiyo haraka iwezekanavyo,” alidokeza Kilavuka.

Website |  + posts
Share This Article