Rais William Ruto aomba pande zote kusitisha vita nchini Israel

Marion Bosire
1 Min Read
Rais William Ruto.

RaiswaKenyaWilliamRuto ameungana na viongozi wa nchi nyingine ulimwenguni katika kusimama na serikali ya Israel wakati huu ambapo nchi hiyo inakumbwa na vita.

Kwenye ujumbe wake Rais Ruto alilaani mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia nchini Israel.

Kiongozi wa nchi aliwasilisha pia ujumbe wa watu wa Kenya ambao alisema wanasimama na wenzao wa Israel na akatoa risala za rambi rambi kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao kwenye mashambulizi yaliyotekelezwa Jumamosi.

“Kenya inashikilia kwamba ugaidi kamwe sio halali na ni tishio kubwa kwa amani na usalama ulimwenguni.” Alisema Rais kwenye ujumbe huo huku akiomba jamii ya kimataifa kuungana katika kukabili watekelezaji wa mashambulizi dhidi ya raia wa Israel na wafadhili wao.

Alisema Kenya ina msimamo sawa na wale ambao wanaotaka pande zote kusitisha vita nchini Israel.

Kundi la Hamas ambalo linadhibiti ukanda wa Gaza lilifanya mashambulizi ya kushtukizia juu ya Israel.

Kamanda wa jeshi la Hamas alisema hatua yao ni ya kulipiza kisasi kwa maovu ambayo Israel imekuwa ikitendea watu katika ukanda wa Gaza.

Sababu nyingine iliyochochea mashambulizi hayo kulingana na ripoti ni kutoheshimiwa kwa msikiti wa Al Aqsa.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza vita huku akiapa kufanya eneo zima la Gaza kuwa mahame.

Share This Article