Rais William Ruto leo Ijumaa, amemteua aliyekuwa waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa digitali Eliud Owalo kuwa naibu mkuu wa wafanyakazi.
Kupitia kwa taarifa, mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei alisema uteuzi wa Owalo, unalenga kufanikisha utathmini na utekelezwaji wa miradi ya serikali kuambatana na mpango wa kuimarisha uchumi wa BETA.
“Uteuzi huu wa kiwaziri miongoni mwa maswala mengine, umejukumiwa kutekeleza kikamilifu na kutathmini miradi na mikakati ya serikali kuambatana na mpango wa BETA,” ilisema taarifa hiyo ya Koskei.
Wakati huo huo, Rais William Ruto amemteua aliyekuwa waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria kuwa mshauri mkuu katika baraza la washauri wa kiuchumi.
Katika uteuzi huo, kiongozi wa taifa alisema hatua hiyo inanuia kuboresha utekelezwaji wa mpango wa uimarishaji wa uchumi wa BETA unaotekelezwa na Baraza jumuishi la Mawaziri.
Rais pia amemteua Dennis Itumbi kuongoza kitengo cha ubunifu wa kiuchumi na miradi maalum katika afisi ya Rais.
Uteuzi wa Itumbi unakusudia kupiga jeki ukuaji wa kiuchumi.