Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi atafanya ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia kesho Jumanne.
Rais Nyusi atapokelewa na mwenyeji wake Samia Suluhu katika Ikulu ya Rais jijini Dar es Salaam atakapowasili nchini humo.
“Rais Samia na mgeni wake Rais Nyusi watashiriki mazungumzo ya pamoja ambayo yatajikita katika sekta ya bishara, uwekezaji, ulinzi na usalama na kisha kushuhudia uwekaji saini wa makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano,” alisema Sharifa Nyanga, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
“Ziara hii itaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kidugu na kidiplomasia baina ya tanzania na Msumbiji ambao uliasisiwa na vongozi wetu; kiongozi wa kwanza wa chama tawala cha nchi hiyo (FRELIMO), Hayati Eduardo Chivambo Mondlane na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere.”
Kadhalika, Rais Nyusi atakuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya 48 ya biashara ya kimataifa mjini Dar es Salaam Jumatano wiki hii.