Rais wa Shirikisho la kandanda barani Afrika, CAF, Dkt. Patrice Motsepe leo Ijumaa anatarajiwa kukagua viwanja vya Kenya vitakavyotumika kwa maandalizi ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani (CHAN) mapema mwakani.
Motsepe aliwasili nchini jana usiku akitokea Dar es Salaam, Tanzania alipofanya ukaguzi sawia.
Alilakiwa na Rais wa FKF Hussein Mohammed alipowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.
Kinara huyo wa CAF atazuru viwanja vya Kasarani, Nyayo, Police Sacco na Ulinzi Sports Complex na kumalizia na JKIA.
Baada ya ukaguzi wake, Motsepe atafanya kikao na wanahabari katika uwanja wa taifa wa Nyayo saa sita unusu adhuhuri.
Hii ni ziara ya pili ya kinara huyo wa CAF humu nchini mwaka huu.
Kenya, Tanzania na Uganda zitaandaa makala ya nane ya kipute cha CHAN kati ya Februari Mosi na 28 mwaka ujao.
Baadaye mwaka 2027, mataifa hayo matatu yatakuwa mwenyeji wa fainali za 36 za Kombe la AFCON.
Ujio wa Motsepe unatarajiwa kuondoa hofu na kutoa hakikisho la Kenya kuandaa fainali za CHAN.