Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewaonya mabalozi wa kigeni dhidi ya kuiingilia maswala ya ndani ya taifa hilo,hususan uchunguzi unaoendelea kuhusu utekaji nyara na mauaji ya wanasiasa wa upinzani.
Bi Samia amewafokea baadhi ya mabolozi wa kigeni walio Tanzania kuhusu matamshi waliyotoa akisema kamwe hatakubali.
Kulingana na kitengo cha 41 cha sheria za Tanzania,mabalozi wa kigeni hawaruhusiwi kuingilia kati maswala ya ndani ya taifa wanakohudumu.
Haya yanajiri kufuatia mauaji ya mwanasiasa wa upinzani wa chama cha Chadema Ali Mohammed Kibao kwa njia tatanishi Septemba 6 mwaka huu.
Samia amesimama kidete kuwa taifa lake halitachukua masharti jinsi ya kuendesha uchunguzi kutoka kwa mabalozi wa kigeni.
Kibao alitekwa nyara kutoka ndani ya basi la umma na watu walioaminika kuwa maafisa wa polisi waliovalia nguo za kiraia na baadaye mwili wake kupatikana kichakani ukiwa na majeraha ya kumwagiwa tindikikali.
Muungano wa ulaya,Ubalozi wa Uingereza ,Ubalozi wa Canada,,Uswizi na Norway zilitoa taarifa ya pamoja tarehe 10 mwezi huu, kulaani mauaji hayo na kutaka uchunguzi wa kina kufanyika.
Ubalozi wa Marekani pia ulipendekeza kufanywa kwa uchunguzi huru na wa haki kuhusiana na utekaji nyara na mauaji hayo.
Joto la kisiasa limependa nchini Tanzania, huku kampeini za uchaguzi zikiendelea mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.