Rais Samia asaidia wanamuziki wawili wakongwe

Wazee hao walipokea shilingi milioni 10 kila mmoja kutoka kwa Rais Samia.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewakumbuka na kuwasaidia wanamuziki wawili wakongwe wanaougua nchini humo.

Rais Samia alimtuma Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, kutembelea na kumjulia hali Mwanamuziki Mkongwe Mzee Hassan Rehani Bichuka nyumbani kwake huko Sinza Mori, Jijini Dar es salaam.

Katika ziara hiyo, Mwinjuma aliwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye amemtakia Bichuka kila la kheri katika kipindi chake cha matibabu na kumuombea apone haraka.

Aidha, Naibu Waziri Mwinjuma amemkabidhi Mzee Bichuka shilingi milioni 10 taslimu, fedha ambazo zimetolewa na Rais Samia kama mkono wa pole na faraja ili kumtia moyo wakati huu anapopitia changamoto za kiafya.

Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alikuwa amemzuru Mwanamuziki Mkongwe wa muziki wa dansi Zahir Ally Zorro nyumbani kwake Kigamboni Jijini Dar es salaam kwa lengo la kumpa pole kutokana na changamoto za kiafya anazopitia.

Hamis Mwinjuma alimkabidhi Zahir Ally Zorro pia shilingi milioni 10 taslimu kama salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan, huku akimtakia kupona haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Akizungumza baada ya kumtembelea Mkongwe huyo, Naibu Waziri Mwinjuma alisema Serikali inaendelea kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Wasanii Wakongwe katika kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania.

Aliosema pia kwamba Wakongwe hao ni hazina muhimu ya Taifa na wanastahili kuenziwa pamoja na kupewa faraja wanapokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya au kijamii.

Share This Article