Rais Samia amwomboleza Grace Mapunda

Marion Bosire
1 Min Read

Kiongozi wa taifa la Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan leo alimwomboleza mwigizaji mkongwe Grace Mapunda aliyefariki baada ya kuugua kwa muda.

Kupitia mitandao ya kijamii Rais aliandika, “Ninatoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wasanii hasa waigizaji wa filamu nchini kwa kuondokewa na ndugu yetu, Grace Mapunda.”

Rais Samia alimsifia marehemu akisema alitumia kipaji chake kwa zaidi ya miaka 20 kutoa burudani na kuelimisha mamilioni ya Watanzania kupitia tamthilia alizoshiriki.

“Mwenyezi Mungu ampumzishe pema na aendelee kuijalia familia yake faraja na subra.” alimalizia Rais Samia.

Leo ndio ilikuwa siku ya safari ya mwisho ya mwendazake Grace ambapo mwili wake ulikifikishwa katika makazi yake huko Sinza Vatican Jijini Dar es salaam mapema asubuhi.

Ibada fupi iliandaliwa huko kabla ya mwili huo na waombolezaji kuelekea uwanja wa Leaders kwa ajili ya kuuaga.

Baadaye jioni mwili huo ulipelekwa katika makaburi ya Kinondoni ambapo unapumzishwa milele.

Mwigizaji huyo mkongwe nchini Tanzania alifariki usiku wa Novemba Mosi, 2024, katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Share This Article