Rais William Ruto amesema serikali yake imetenga shilingi bilioni 2.7 za kuinua sekta ya uvuvi kote nchini huku eneo la Pwani likitengewa shilingi bilioni 1.2.
Akizungumza wakati wa sherehe za Mashujaa katika uwanja wa Kwale, Ruto amesema analenga kuhakikisha uchumi wa baharini unachangia shilingi bilioni 80 kila mwaka kwa Pato Ghafi la Taifa katika muda wa miaka mitano ijayo.
Uchumi wa bahari kwa sasa unachangia Pato Ghafi la Taifa la shilingi bilioni 20 kila mwaka.
Kulingana na Ruto, pesa hizo zitatumika kujenga viwanda vidogo vya kuhifadhi samaki kwa barafu na kununua vifaa vya uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi nchini.
Aidha serikali imetenga ruzuku ya shilingi bilioni 1.7 kwa vyama vya ushirika 612 na makundi ya uvuvi katika eneo la Pwani.
Rais ameongeza kuwa kufaulu kwa uchumi wa baharini kutabuni maelfu ya nafasi za ajira na kuinua uchumi wa taifa.