Rais Ruto: Wabunge wamefanya kazi maridhawa

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amewapongeza wabunge kwa kufanya kazi pamoja katika kuunga mkono ajenda ya serikali katika bunge la Seneti la lile la Kitaifa. 

Alitaja kupitishwa kwa miswada ya fedha na upatikanaji wa afya kwa wote akisema ni baadhi ya sheria muhimu zitakazosaidia katika kutatua changamoto zinazowakumba Wakenya.

“Lazima niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya katika kupitisha miswada ya serikali inayolenga kubadilisha maisha ya watu wetu punde itakapotekelezwa,” alisema Rais Ruto.

Aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa wabunge wa bunge la Seneti la lile la Kitaifa uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.

Aliwataka wabunge hao kuwa tayari kupitisha miswada zaidi ambayo itawasilishwa katika mabunge yote mawili hivi karibuni.

Alisema miswada juu ya utakatishaji fedha, kipindi cha kati juu ya mkakati wa mapato na utangazaji wa mali na mgongano wa maslahi hivi karibuni itawasilishwa katika mabunge yote mawili ili kuidhinishwa.

Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa wito kwa wabunge hao kuwaelimisha watu katika maeneo bunge yao husika kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kuangazia changamoto zinazowakumba.

Kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Aaron Cheruiyot na mwenzake wa bunge la Taifa Kimani Ichung’wa waliupongeza uongozi wa Rais Ruto wakiutaja kuwa shirikishi.

Share This Article