Rais William Ruto amesema Serikali ina nia ya kuongeza akiba ya nchi hii.
Kiongozi wa taifa alisema hatua hiyo itaiondolea nchi haja ya kukopa kutoka nje, jambo ambalo limedumaza uchumi.
Alibainisha kuwa nchi ilikuwa imeweka akiba Shilingi bilioni 350 pekee katika kipindi cha miaka 60 kwenye Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).
Hata hivyo, alieleza kuwa Serikali imebadili mwenendo huo na iko mbioni kuongeza maradufu akiba ya NSSF ndani ya miaka minne.
“Kwa muda mfupi, hatutahitaji kukopa kutoka mahali pengine kukuza uchumi wetu,” alisema Rais.
Aliyasema hayo siku ya Jumapili wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la Faith Evangelistic Ministry huko Karen, Kaunti ya Nairobi.
Mke wa Rais Rachel Ruto, Waziri wa Mazingira Soipan Tuya, Magavana Anne Waiguru na Susan Kihika pia walihudhuria ibada hiyo.
Rais Ruto alisema hatua za Serikali zinazolenga kupunguza gharama ya maisha zinazaa matunda.
Alisema mpango wa mbolea ya ruzuku umesaidia nchi kuinua uzalishaji wa chakula.
“Matarajio yetu mwaka huu ni kwamba tutaongeza uzalishaji wa mahindi kutoka magunia milioni 44 hadi magunia milioni 61,” alisema.
Rais alisema Serikali ina nia ya kuongeza ekari za ardhi inayotumika kwa kilimo kupitia umwagiliaji wa maji.
Aliongeza kuwa nchi haitatumia tena Shilingi bilioni 500 kila mwaka kuagiza chakula kutoka nje.
“Hatupaswi kuagiza chakula kutoka nje; tunapaswa kuzalisha zaidi na hata kuuza nje cha ziada,” alisema.
Alisema Serikali imeweka mikakati ya makusudi kukabiliana na ukosefu wa ajira.
“Mradi wa nyumba unahusu zaidi nafasi za ajira kuliko nyumba,” alisema.