Rais William Ruto amesema hali ya kutoweka na utekaji nyara wa watu, hauna nafasi yoyote hapa nchini.
Akihutubia taifa katika majengo ya bune leo Alhamisi, alisema licha ya madai mengi kuwa watu walitoweka wakati wa maandamano dhidi ya serikali, baadhi ya visa hivyo vimesuluhishwa huku vingine vikibainishwa kuwa habari za uongo na hivyo kutatiza juhudi za kubainisha visa halisi vya watu waliotoweka.
“Ninalaani hatua zozote za utumizi wa nguvu kupita kiasi ambao huhatarisha maisha ya watu, ikiwa ni pamoja na kupotea na kuhatarishwa kwa maisha,” alisema Rais Ruto.
Alitoa wito kwa wananchi walio na habari kuhusu visa vya kutekwa nyara kwa watu, kuziwasilisha kwa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI na halmashauri ya kutathmini utendakazi wa polisi IPOA iwapo maafisa wa polisi wanadaiwa kuhusika.
“Ninafahamu kuwa nyingi ya kesi hizo zinashushughulikiwa na halmashauri ya kutathmini utendakazi wa polisi IPOA, hatua muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji na haki,” aliongeza kiongozi wa taifa.
Rais hata hivyo alisema kuwa licha ya maandamano kuwa ya kisheria na halali kuambatana na katiba, wakenya wanafaa kujihadhari na wahalifu wanaoingilia maandamano ya amani na kuhatarisha uhuru na usalama wa umma.