Serikali itawachukulia hatua kali wanaotumia vibaya Katiba na kusababisha machafuko hapa nchini.
Rais William Ruto amesema mpango huo utasitishwa. huku akibainisha kuwa Serikali ina wajibu wa kikatiba wa kudumisha sheria na utulivu.
Rais aliwahakikishia Wakenya kwamba Serikali italinda maisha na mali zao. Alisema licha ya kwamba Upinzani una haki ya kikatiba ya kushawishi wengine kufanya mambo fulani, hawana haki ya kusababisha fujo na kuwadhuru Wakenya.
“Hatuwezi kuendelea kutumia maandamano kuharibu mali, biashara na kusababisha vifo,” alisema.
Alieleza kuwa kila rasilimali itatumiwa ili kulinda maisha na mali ya kila Mkenya.
Kiongozi wa taifa alisema hayo siku ya Jumamosi katika kaunti ya Homa Bay, wakati wa hafla ya kutoa shukrani ya Katibu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo.
Rais pia alikabidhi basi na kufungua Maabara ya Ujuzi wa Kidijitali katika shule hiyo.
Viongozi waliokuwepo kwenye hafla hiyo ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri Eliud Owalo (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), Kindiki Kithure (Usalama wa Ndani), Rebecca Miano (Afrika Mashariki), Peninah Malonza (Utalii) na Florence Bore (Leba), Makatibu Wakuu na Wabunge kadhaa.
Rais alisema Serikali itahudumia Wakenya wote kwa usawa na kufanya kazi na viongozi wote bila kujali msimamo wao wa kisiasa. Alisema Serikali ina nia ya kujenga nchi moja yenye umoja isiyo na ukabila na migawanyiko.
Alisema utawala wa Kenya Kwanza hautaruhusu sehemu yoyote ya nchi kuachwa nyuma katika masuala ya maendeleo.
Alisema kila eneo litapata sehemu yake nzuri ya keki ya taifa.
“Tunataka kuhakikisha kuwa tunaondoa siasa za kutengwa na kubaguliwa kwa baadhi ya sehemu za nchi. Tutaiendeleza nchi hii kwa pamoja,” alisema.
Rais alisema Serikali imeweka mikakati thabiti kukabiliana na changamoto zinazowakabili Wakenya, akitaja gharama ya maisha na ajira.
“Katika bajeti hii, tunakusudia kubuni nafasi za ajira,” alisema.
Alisema nchi inaelekea kuwa na mavuno mengi yatakayomaliza uhaba wa chakula nchini kutokana na mbolea ya ruzuku ya Serikali.
Rais alisema Serikali haitaruhusu uingizaji wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa humu nchini ili kutoa fursa kwa Wakenya.
Rais Ruto aidha alisema upinzani hautavuruga ajenda ya maendeleo ya Serikali kupitia maandamano.
“Ninataka kuwaahidi watu wa Kenya kwamba tunasonga mbele na ajenda yetu ya maendeleo,” alisema.