Rais William Ruto amesema kwamba yuko tayari kupambana na washindani wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza alipokamilisha ziara yake ya eneo la mlima Kenya jana huko Othaya, kaunti ya Nyeri Rais alisema pia kwamba yuko tayari kwenda nyumbani mwaka 2027 iwapo hatakuwa ametimiza matarajio ya wakenya.
Kiongozi wa nchi hata hivyo alidhihirisha imani kwamba wakenya watamchagua tena kutokana na mipango yake ya maendeleo ambayo anaamini itabadili utajiri wa nchi hii.
Kwa mara nyingine kiongozi huyo alipuuza wapinzani wake akisema kwamba wapiga kura watachagua wawakilishi wao kwa misingi ya mipango yao ya maendeleo.
Aliwataka wakosoaji wake wampe muda atekeleze ahadi alizotoa kwa wakenya, huku akishauri viongozi wa kaunti ya Kiambu kukomesha malumbano na badala yake waangazie kuhudumia watu wao.
Rais Ruto alisema wiki hii serikali imetoa shilingi bilioni 3.6 zitakazotumiwa kukamilisha miradi mbali mbali ya barabara.
Ruto alisema juhudi za serikali za kuimarisha uchumi na kuimarika kwa thamani ya sarafu ya Kenya kumetoa fursa ya ufadhili na kukamilishwa kwa miradi iliyokuwa imekwama ya barabara.
Kuhusu sekta ya kilimo, kiongozi wa nchi alisema serikali imewekeza pakubwa akiongeza kwamba mpango wa mbolea ya ruzuku umeafikia matarajio ya wakulima.
Kulingana naye mpango huo umeimarisha uzalishalishaji wa chakula na hivyo kusababisha kupungua kwa bei za vyakula na gharama ya maisha kwa jumla.