Rais William Ruto amesema kuwa Serikali itafanya lolote iwezalo kukabiliana na ukosefu wa usalama katika Kaunti ya Lamu.
Alisema hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya wanaochochea watu dhidi ya wenzao.
Rais alibainisha kuwa magaidi wamekuwa wakitumia mgawanyiko huo kuendeleza ajenda yao mbaya.
Aliwaomba viongozi kutoka eneo hilo kujitokeza, kuungana na kufanya kazi kwa pamoja.
“Ni lazima tuilinde Lamu; watu lazima waishi kwa amani kwa sababu wanastahili hivyo,” alisema.
Aliyasema hayo siku ya Alhamisi wakati wa mkutano na viongozi kutoka Kaunti hiyo katika Ikulu ya Nairobi.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) na Aden Duale (Ulinzi), Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo, Gavana wa Kaunti ya Lamu Issa Timamy, wabunge Ruweida Obbo (Lamu Mashariki), Stanley Muthama (Lamu Magharibi), Joseph Githuku (Seneta, Lamu), Monica Muthoni (Mwakilishi wa Wanawake, Lamu) na Wawakilishi wa Wadi walikuwepo.
Kiongozi wa Nchi alisema kuwa Serikali ina nia ya kuhakikisha kaunti hiyo itafungua uwezo wake wa kiuchumi, akitoa mfano wa biashara ya bandari ya eneo hilo.
Aliahidi kushughulikia umiliki wa ardhi na changamoto za maskwota zinazokabili Kaunti hiyo.
“Tutajenga nyumba za bei nafuu, tutaweka maeneo ya wavuvi kupakulia samaki, tutaanzisha vituo vya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari, tutaanzisha Hifadhi za Kukuza Viwanda na kuifanya bandari kuwa ya kibiashara ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi,” alisema.
Alisema watakaohujumu mipango hiyo ya kuleta mabadiliko ni maadui wa wananchi.